Mayai Sijemaliza
Fuga kuku mechagua, kuku wa yetu asili,
Mayai wajizolea, kula jenga wako mwili,
Kuku kwa yai tokea, nayo ndani yake mwili,
Mayai sije maliza, kaja kosa kuja taga.
Kaja kosa kuja taga, kisa hakuna uzao,
kwa mikogo kajikaga, kitafuna chote leo,
badae takuja bwaga, na sipate kimbilio.
Mayai sije maliza, kaja kosa kuja taga.
Sitake ionja sumu, kwa maziwa siyonayo,
Hospitali kugumu, takosekana tibayo,
Kodoa nalo jukumu, uone yarefushwayo,
Mayai sije maliza, kaja kosa kuja taga.
Kisa moto kuwashia, sitoe yote makuti,
Kivuli kakupotea, na amani sije keti,
Usambe sikukwambia, sing’amue tofauti,
Mayai sije maliza, kaja kosa kuja taga.
Liuza maziwa pupa, leo ndama twatabika,
Tabika kitoka kapa, maziwa yanamashaka,
mashaka kwa zao pupa, livyojalia Rabuka
Mayai sije maliza, kaja kosa kuja taga.
Wanotumia wa moza, vya kwao sijevimwaga,
Nia mifugo ongeza, mayai tele kitaga,
Ya ndani mekueleza, mfanowe nawe iga,
Mayai sije maliza, kaja kosa kuja taga.
Copyright © Mussa Shikome | Year Posted 2018
Post Comments
Poetrysoup is an environment of encouragement and growth so only provide specific positive comments that indicate what you appreciate about the poem. Negative comments will result your account being banned.
Please
Login
to post a comment